Вход на сайт

Просмотр новости

Найдите то, что Вас интересует

Mpinzani wa Hichilema ashikiliwa kwa tuhuma za uhaini

Дата публикации: 28-08-2026 11:53:43

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile na mgombea mwenza wake, Makebi Zulu wamewekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa tuhuma zinazohusishwa na uhaini, hatua inayoongeza mvutano wa kisiasa baada ya uchaguzi wa Agosti 13, 2026 uliompa Rais Hakainde Hichilema ushindi wa muhula wa pili.

Основное содержимое страницы с новостью.

Ijumaa, Agosti 28, 2026

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile aliyenyoosha mikono

Muktasari:
  • Brian Mundubile amejisalimisha polisi Agosti 27 baada ya wito wa Agosti 20, kufuatia tuhuma za kutishia usalama wa Taifa, huku akikanusha madai hayo na kupinga matokeo ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile na mgombea mwenza wake, Makebi Zulu wamewekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa tuhuma zinazohusishwa na uhaini, hatua inayoongeza mvutano wa kisiasa baada ya uchaguzi wa Agosti 13, 2026 uliompa Rais Hakainde Hichilema ushindi wa muhula wa pili.

Jeshi la Polisi nchini humo jana Alhamisi, Agosti 27, lilithibitisha kuwashikilia viongozi hao baada ya kuripoti na kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazohusishwa na usalama wa Taifa.

Polisi walisema wawili hao walihojiwa na kupewa taarifa kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao baada ya uchunguzi kukamilika, ingawa hawajaweka wazi kwa undani tuhuma zinazowakabili.

Mundubile aliyekuwa mgombea wa National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP), alijisalimisha kwa polisi jana baada ya kukaa mafichoni kwa takriban wiki mbili na kupata hifadhi katika jengo la Umoja wa Mataifa mjini Lusaka.

Hatua hiyo ilifuatia wito wa polisi uliotolewa Agosti 20, 2026, ukiwataka Mundubile na Zulu kufika kwa mahojiano kuhusu madai ya vitisho kwa usalama wa Taifa.

Hata hivyo, Mundubile amekanusha tuhuma hizo, akisema ni za kisiasa. Pia amekanusha madai kwamba alikuwa akipanga uasi au kuunda kikundi cha kijeshi.

Tukio hilo linafuatia operesheni ya vikosi vya usalama nchini humo, ambapo polisi walisema walikabiliana na watu waliokuwa na silaha na kuwakamata watu 11. Serikali ilisema operesheni hiyo ilihusishwa na tishio kwa usalama wa Taifa na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mutotwe Kafwaya.

Matokeo yaliyokataliwa

Mundubile alikuwa mshindani mkuu wa Hichilema katika uchaguzi wa Agosti 13, 2026, ambao Rais huyo alitangazwa mshindi kwa kupata kura 2,965,326, sawa na asilimia 61.4, huku Mundubile akipata kura 1,856,217, sawa na asilimia 38.

Hichilema alitangazwa rasmi mshindi Agosti 18, lakini Mundubile alikataa matokeo hayo, akidai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na kutokuwiana katika uendeshaji, uhesabuji, usafirishaji na utangazaji wa matokeo.

Alitangaza kukata rufaa mahakamani, lakini hatua hiyo ilikumbana na kikwazo Agosti 24, siku ya mwisho ya kikatiba ya kuwasilisha pingamizi la matokeo ya urais.

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile alipokuwa anapiga kura uchaguzi mkuu Zambia.

Siku hiyo, mahakama nchini Zambia zilifungwa na kuzungushiwa ulinzi wa polisi. Inadaiwa waraka wa uongozi wa Mahakama uliwataka wafanyakazi kutofika kazini kutokana na hofu za kiusalama zilizotokana na mvutano wa uchaguzi.

Human Rights Watch (HRW) ililaani hatua hiyo, ikisema Katiba ya Zambia inataka pingamizi dhidi ya matokeo ya urais liwasilishwe ndani ya siku saba.

Kwa kuwa Hichilema alitangazwa mshindi Agosti 18, Agosti 24 ilikuwa siku ya mwisho kwa Mundubile kuwasilisha pingamizi lake.

HRW ilisema kufungwa kwa mahakama kulizuia upatikanaji wa haki kwa Mundubile na wengine waliotaka kupinga matokeo.

Chishala Kateka, kiongozi wa New Heritage Party na mshirika wa Mundubile alisema walikuwa wakifanya kila walichoweza kuhakikisha madai ya Mundubile yanafikishwa mahakamani.

Baadaye, taarifa zilieleza kuwa Mahakama ilithibitisha kupokea hati iliyotumwa kwa barua pepe binafsi ya Jaji Mkuu Mumba Malila na kuipeleka Mahakama ya Katiba kuamua iwapo ilikuwa imewasilishwa kihalali. Hata hivyo, haikuwa wazi ikiwa hati hiyo ilikuwa pingamizi rasmi la Mundubile lililowasilishwa kwa utaratibu wa kawaida wa Mahakama.

Waangalizi wa uchaguzi

Umoja wa Ulaya ulisema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani, lakini uwanja haukuwa sawa kikamilifu kutokana na vikwazo vya kampeni na faida iliyokuwa upande wa chama tawala.

EU pia ilisema kulikuwa na matukio makubwa ya ukiukwaji wa taratibu wakati wa kuhesabu na kujumlisha kura, hali iliyoathiri uwazi na uaminifu wa mchakato.

Umoja wa Mataifa nao umeonyesha wasiwasi kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa viongozi wa upinzani baada ya uchaguzi.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Turk, ametaka hatua za kisheria dhidi yao zifuate sheria za Zambia na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Kukamatwa kwa Mundubile na Zulu kunatokea wakati Zambia ikiendelea na maandalizi ya kumuapisha Hichilema kwa muhula wake wa pili, huku mvutano kuhusu matokeo ya uchaguzi ukiendelea.

Схожие новости

#Наименование новостиТональностьИнформативностьДата публикации
1Zambia: Hakainde Hichilema expected to win upcoming vote08.413-08-2026
2The Zambian government has arrested the main opposition leaders on the very night of the elections04.2617-08-2026
3Zambia heads to polls with President Hichilema expected to win second term06.6913-08-2026
4Zambian opposition leader detained011.0228-08-2026
5Zittende president Zambia zoals verwacht herkozen09.318-08-2026
6Hichilema rallies thousands as Zambia heads to presidential vote07.9412-08-2026
7Zambia: Arrests and detention of political opponents following election raises concern0919-08-2026
8Президента Замбии переизбрали на второй срок014.9318-08-2026
9Samia Suluhu Hassan Hails Hichilema's Zambia Re-Election Victory013.6719-08-2026
10Hivi ndivyo Dk Nchimbi anavyoweza kurudi CCM01027-08-2026

Классификация: Информация. Схожих патентов: 0. Схожих новостей: 10. Тональность: 0. Информативность: 8.9. Источник: www.mwananchi.co.tz.