Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu katika kuvutia wawekezaji nchini Tanzania kwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika unaohitajika katika shughuli za uzalishaji.
Alhamisi, Agosti 27, 2026

Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu katika kuvutia wawekezaji nchini Tanzania kwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika unaohitajika katika shughuli za uzalishaji.
Uwepo wa nishati ya kutosha ni moja ya vigezo muhimu kwa wawekezaji, hasa wanaolenga kuanzisha viwanda, migodi, shughuli za kilimo cha kibiashara na biashara zinazotumia teknolojia.
Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kituo hicho Agosti 22, 2026, Rufiji mkoani Pwani, huku Wizara ya Nishati ikisema mradi huo umegharimu Sh7.452 trilioni na hadi Mei 31, 2026 ulikuwa umechangia asilimia 44.9 ya umeme wote ulioingia kwenye Gridi ya Taifa ndani ya mwaka mmoja.
Uwezo wa JNHPP kuzalisha megawati 2,115 unaongeza nguvu ya Tanzania katika kuhakikisha mahitaji ya ndani ya umeme yanakidhiwa na kuwa na ziada kwa ajili ya shughuli nyingine za kiuchumi.
Hali hiyo inafungua fursa kwa wawekezaji kuanzisha viwanda karibu na maeneo yenye malighafi bila hofu kubwa ya kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati.

Kwa Tanzania inayolenga kujenga uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, umeme wa uhakika unaweza kuwa sehemu muhimu ya mazingira ya uwekezaji.
Zaidi ya kuongeza uzalishaji, nishati hiyo inaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao, kuchochea uanzishwaji wa biashara mpya na kuongeza ajira. Hivyo, JNHPP si mradi wa kuongeza umeme pekee, bali ni miundombinu inayoweza kubadili uwezo wa Tanzania kuvutia mitaji na kuongeza uzalishaji wa ndani.
Akizungumzia kuzinduliwa kwa mradi huo, Mchambuzi wa Biashara na Uchumi, Aurelia Kamuzora anasema uwepo wa Bwawa la Mwalimu Nyerere utasaidia kuongeza uzalishaji, kuchochea ujenzi wa viwanda kuvutia wawekezaji wanaotegemea umeme katika uzalishaji hivyo kuchangia kufikia lengo la kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Anasema umeme ni muhimu katika uzalishaji kama ilivyo mishipa katika mwili wa binadamu, hivyo upatikanaji wa umeme wa uhakika utawezesha viwanda vikubwa na vidogo kuongeza uzalishaji.
Anasema uchumi unategemea uzalishaji na kwa kuwa uzalishaji mwingi unahitaji umeme, ni muhimu kuhakikisha huduma hiyo inafika maeneo yote, hususan vijijini ambako kuna malighafi nyingi zinazoweza kuchakatwa na kuongeza thamani.
“Viwanda vidogovidogo hatuwezi kuwa navyo kama nguvu ya umeme itaelekezwa zaidi mijini. Umeme ukifika vijijini, ambako kuna malighafi na watu wengi, tutaweza kuwafikia zaidi na kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo,” anasema.
Anaongeza kuwa maeneo ya vijijini yana rasilimali kama mazao na miti ambazo zinaweza kutumika kuzalisha bidhaa na kuongeza kipato, lakini ili hilo lifanyike kwa ufanisi, upatikanaji wa umeme ni muhimu.
Kwa mfano, anasema wabunifu na wajasiriamali wanaotumia mashine kuchakata na kusaga mbegu wanaweza kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa zao endapo watapata umeme wa uhakika.
Anasema Bwawa la Mwalimu Nyerere lilibuniwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme ili kuiwezesha Tanzania kuzalisha kwa kiwango kikubwa zaidi, kupata ziada ya bidhaa na hatimaye kuuza nje ya nchi.

Anasema uzalishaji huo ukienda sambamba na uwekezaji katika viwanda na uchakataji wa malighafi, utaongeza thamani ya bidhaa za ndani, ajira na mapato, hatua ambazo zitachangia katika kufikia malengo ya uchumi ya Tanzania ya mwaka 2050.
Haya yanaelezwa wakati takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2021 miradi ya uwekezaji iliyokuwa imesajiliwa ilikuwa 252, ambayo iliongezeka hadi kufikia 293 (2022), miradi 526 mwaka 2023 na 901 mwaka jana kabla ya kufikia miradi 915 mwaka huu.
Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude anasema bwawa hilo ni kichocheo cha kufikia uchumi unaotamaniwa na Tanzania, pamoja na kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Anasema kuzinduliwa rasmi kwa bwawa hilo ni hatua kubwa katika kuiweka Tanzania miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa umeme, hivyo ni muhimu kuhakikisha uwepo wa umeme huo unakuwa na maana kwa uchumi wa nchi.
Anasema kinachopaswa kufanyika sasa ni kujenga miundombinu itakayosaidia kusafirisha umeme kutoka eneo unapozalishwa na kuwawezesha wawekezaji kuutumia ili shughuli za uzalishaji ziweze kufanyika kwa haraka.
“Hili likifanyika ni kuanza kutengeneza uhitaji ili umeme uweze kutumika, kwani Tanzania mahitaji makubwa ya umeme yaliyowahi kufikiwa ni kama megawati 2,100. Sasa kama una umeme wa megawati 4,400 unakuwa na akiba kubwa ambayo huna matumizi nayo,” anasema.
Anasema ili kutengeneza mahitaji hayo ni vyema kuangalia namna ya kuuza umeme huo katika masoko ya kikanda, jambo ambalo linapaswa kwenda sambamba na kuongeza matumizi ya ndani kwa kupanua shughuli za uzalishaji, ikiwamo kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na shughuli nyingine zitakazofanya umeme uhitajike.
“Tukiweza kupanua sekta ya uzalishaji kama viwanda na shughuli nyingine, tutaona kupanda kwa uzalishaji. Uzalishaji ukipanda kwa kuongeza ufanisi utafanya tupate fedha na namna nyingine ni viwanda kupanuka. Hizi zote tutakuja kuona kwa pato la Taifa kukua,” anasema.
Anasema hatua hiyo itasaidia sekta ya viwanda kukua, kutengeneza ajira na kuwezesha mitaji na ardhi kutumika kwa namna inayopaswa.
Anasema haya yote yanapaswa kufanyika kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuhakikisha malalamiko ya wawekezaji yanafanyiwa kazi na kuondolewa, hivyo kuwapa wawekezaji uhuru wa kuweka mitaji yao.
Kuhusu njia za usambazaji alizosema Mkude tayari lilitolewa ufafanuzi na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi ambaye alieleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme ili kuhakikisha ongezeko la uzalishaji, hususan kutoka katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), linafika kwa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ndejembi anasema kuongeza uwezo wa uzalishaji pekee haitoshi bila kuwa na mtandao imara wa kusafirisha umeme.
"Rais Samia, hata hivyo, tunatambua kuongeza uwezo wa uzalishaji pekee haitoshi. Lazima tuwe na mtandao wenye uwezo wa kupokea na kusafirisha umeme wote kwenda maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” anasema Ndejembi.
Awali, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange anasema kituo kituo hicho ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya umeme na tayari kinaonyesha matokeo kupitia mchango wake katika gridi ya taifa.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) Agosti 22, 2026, Rufiji mkoani Pwani,
Anasema kituo kilianza kuzalisha umeme Februari 2024 baada ya shirika hilo kupokea mtambo wa kwanza kutoka kwa mkandarasi.
“Mwaka 2025 kituo hiki kimechangia asilimia 43.5 ya umeme wote ulioingizwa kwenye gridi. Na mwaka huu kituo kimechangia nusu ya umeme wote ulioingia kwenye gridi ya taifa,” anasema.
Anasema takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa kituo hicho katika kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka kwa kasi nchini.
“Takwimu hizi zinaonyesha wazi kabisa kwamba kituo cha Julius Nyerere tayari kimekuwa mhimili mkubwa kabisa wa nishati na kimeboresha sana hali ya upatikanaji wa umeme wa taifa letu,” anasema.
| # | Наименование новости | Тональность | Информативность | Дата публикации |
|---|---|---|---|---|
| 1 | MBEGU YA UCHUMI: Kugeuza umeme wa ziada kuwa fursa ya kiuchumi | 0 | 7.3 | 27-08-2026 |
| 2 | China kuisaidia Tanzania usimamizi mashirika ya umma | 0 | 4.56 | 26-08-2026 |
| 3 | Bunge lafuta Tasnia ya Pareto | 0 | 7.71 | 28-08-2026 |
| 4 | Mo Dewji asaka fursa za uwekezaji Botswana | 0 | 6.55 | 27-08-2026 |
| 5 | Waliopata ajira mtandaoni kupatiwa mikopo | 0 | 9.33 | 27-08-2026 |
| 6 | Stanbic benki yarahisisha malipo ya Shilingi China | 0 | 5.72 | 28-08-2026 |
| 7 | Songwe waanza mpango wa kutokomeza utoro shuleni | 0 | 4.68 | 27-08-2026 |
| 8 | Глава ТПП считает, что меры поддержки бизнеса смягчат негативные тенденции в экономике | 0 | 0 | 31-03-2020 |
| 9 | Мишустин поручил выделить больше средств на технопарки в следующие три года | 0 | 0 | 04-06-2025 |
| 10 | Путин назвал жизненно важным для России опережающее развитие обрабатывающей промышленности | 0 | 0 | 04-04-2023 |