Soma zaidi hapa...
Prime
Jumatatu, Agosti 10, 2026
Dar/Morogoro. Baadhi ya shule mkaoni Morogoro zimefungwa kwa muda kupisha maandalizi na uendeshaji wa mashindano ya shule za Afrika Mashariki (Feassa), yanayofanyika mkoani humo.
Hatua hiyo imeibua hofu kwa baadhi ya wazazi kuhusu athari za kusitishwa kwa masomo, hasa kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani, pamoja na namna muda wa masomo uliopotea utakavyofidiwa.
Kuanzia Julai 24, baadhi ya shule za msingi na sekondari za Morogoro Mjini zilifungwa na zinatarajiwa kufunguliwa tena Agosti 24, huku mashindano hayo yakitarajiwa kuanza Agosti 12-23.
Mashindano hayo huwakutanisha wanafunzi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ambapo michezo mbalimbali hufanyika ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, wavu, kikapu na riadha.
Miongoni mwa shule hizo zilizofungwa Kikundi, mafiga, Kihonda maghorofani, Juhudi, Kambi tano, Lukobe, Uhuru, Azimio, Chamwino, Kilongo, St Peter’s Seminary na Morogoro Sekondari.
Baadhi ya wazazi wamehoji uamuzi huo, wakitaka kujua namna vipindi vilivyokosa kufundishwa vitakavyofidiwa, wakati wanafunzi katika maeneo mengine nchini wakiendelea na masomo kama kawaida.
“Bora ratiba ya mashindano haya ingekuwa kipindi cha likizo, lakini hivi sasa masomo yanaendelea, wanafunzi wa shule za Morogoro wapo nyumbani, si sawa, hususan kwa wale wa madarasa ya mitihani,” amesema mzazi mmoja mwenye watoto wanaosoma Kidato cha pili na cha nne Morogoro Sekondari.
Mzazi mwingine, aliyeomba hifadhi ya jina amesema mwanawe wa kidato cha pili aliyekuwa bweni alirejeshwa nyumbani baada ya shule kufungwa, hatua iliyomlazimu kumtafutia masomo ya ziada.
“Nilipigiwa simu Julai 26 nitume nauli kwa sababu shule zimefungwa, nikauliza sababu nikaambiwa ni kupisha mashindano ya Feassa, nilishangaa tangu lini mambo haya, lakini ndiyo utaratibu wao, sikuwa na namna,” amesema.
Baadhi ya walimu wakuu wa shule zilizofungwa, walipoulizwa kuhusu athari za hatua hiyo kwa wanafunzi, hususan wa madarasa ya mitihani, walisema athari zinaweza kudhibitiwa iwapo shule zitajipanga kufidia muda uliopotea.
“Kama shule ambazo watoto wapo nyumbani zitajipanga vizuri watakaporudi, hakutakuwa na tatizo, kwa upande wetu, tumeamua likizo ya Septemba watoto hawatofunga ili kufidia siku hizi ambazo wapo nyumbani,” amesema mmoja wa walimu wakuu akiomba hifadhi ya jina lake.
Kauli ya Kamishna wa Elimu
Leo Jumatatu, Agosti 10, 2026, Mwananchi limemtafuta Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahaba kuhusu utaratibu huo wa shule za Mjini Morogoro kufungwa awali alihoji ni kwa vipi zimefungwa wakati yeye hajatoa waraka huo.
Hata hivyo, aliomba apewe muda kulifuatilia hilo na baada ya nusu saa akaiambia Mwananchi amefuatilia kwa Morogoro ni kweli shule zimefungwa ili kupisha mashindano ambapo yatafanyikia mkoani humo.
"Kule kuna sekretarieti ambayo inaratibu mashindano hayo, ungekuwa Morogoro muda huu ungekwenda kuzungumza nayo wakupe taarifa zaidi, lakini nimewasiliana nao na wamenieleza kuwa ni utaratibu wa kawaida wa mashindano hayo," amesema.
Amesema wanafunzi ambao watakosa masomo kwa kipindi hiki watafidiwa watakaporejea shuleni.
Awali, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, Euphrasia Buchuma, alikiri baadhi ya shule mkoani humo kufungwa kipindi hiki.
Alipoulizwa sababu za shule hizo kufungwa na namna muda wa masomo utakavyofidiwa kwa wanafunzi alisema kwa kifupi zimefungwa kupisha mashindano ya Feassa.
"Si shule zote zimefungwa," amesema Buchuma bila kufafanua utaratibu wa kufidia muda wa masomo kwa wanafunzi walioko nyumbani na kubainisha wale wa darasa la saba wenyewe kutofunga.
“Wanafunzi wa darasa la saba wana mitihani next month (mwezi ujao), hao watafungaje?” amesema Buchuma.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu athari hasi kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani mengine, ikiwamo darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne, alikata simu, alipopigiwa tena hakupatikana.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-Tamisemi), Adolf Nduguru alipoulizwa kuhusu kufungwa kwa shule hizo mkoani Morogoro alisema suala hilo linapaswa kufafanuliwa na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Dk Mussa Ali Mussa.
Hata hivyo, Dk Mussa alipopigiwa simu yake iliita mara kadhaa bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.
Mwananchi pia ilimtafuta Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima ambaye simu yake iliita bila kupokelewa huku mkuu wa wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala akidai hana hizo taarifa na kutaka aulizwe Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Morogoro, Emmanuel Mkongo ambayealipotafutwa simu yake pia iliita bila kupokelewa
Meya wa Manispaa ya Morogoro, Khalid Matengo akibainisha kuwa na taarifa za kufungwa shule hizo lakini yeye hayuko kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo kwa sababu michezo hiyo inaratibiwa na mkoa, hivyo mwenye nafasi na mamlaka ya kulizungumzia hilo ni mkuu wa mkoa.
Akizungumzia mashindano hayo, ofisa michezo wa Morogoro, Grace Njau, amesema maandalizi yanaendelea na Agosti 12 washiriki kutoka nchi mbalimbali watawasili, kabla ya michezo kuanza rasmi Agosti 14 katika viwanja mbalimbali.
Alisema ufunguzi rasmi wa mashindano hayo utafanyika Agosti 16 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ukitarajiwa kuongozwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
| # | Наименование новости | Тональность | Информативность | Дата публикации |
|---|---|---|---|---|
| 1 | Ongezeko la wahitimu wa vyuo, wadau watoa pendekezo | 0 | 10 | 10-08-2026 |
| 2 | Hivi ndivyo mwanachuo anaweza kujiajiri | 0 | 10 | 12-08-2026 |
| 3 | Migogoro inapogeuka rafiki wa ndoa | 0 | 10 | 09-08-2026 |
| 4 | Ijue siri ya kisukari iliyojificha kwenye wali, ugali | 0 | 10 | 07-08-2026 |
| 5 | Резидент ТОР "Надеждинская" построит школу на условиях государственно-частного партнерства | 0 | 0 | 05-03-2021 |
| 6 | Mahitaji ya huduma za moyo Comoro yaipa fursa JKCI | 0 | 5.4 | 12-08-2026 |
| 7 | В дагестанском селе Оружба построили новую школу на 304 места | 0 | 0 | 18-12-2021 |
| 8 | Власти Северной Осетии сообщили, что новую школу построят в Моздоке до конца 2019 года | 0 | 0 | 15-08-2019 |
| 9 | В Моздоке открыли школу на 500 мест | 0 | 0 | 30-11-2020 |
| 10 | Адыгее выделили более 1,3 млрд рублей на строительство трех новых школ | 0 | 0 | 20-12-2021 |