Вход на сайт

Просмотр новости

Найдите то, что Вас интересует

Mnyika ajitwisha dhamana mkutano Lissu aliodaiwa kufanya uhaini

Дата публикации: 28-08-2026 16:22:30

Soma hapa...

Основное содержимое страницы с новостью.

Muktasari:
  • Ushahidi wa Mnyika ni wa pili katika utetezi wa Lissu, baada ya mshtakiwa huyo kuhitimisha ushahidi wa msingi leo Agosti 28, 2026.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ameeleza mahakamani kubeba dhamana ya mkutano ambao Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu anatuhumiwa kuutumia kutenda kosa la uhaini, akisema yeye ndiye aliyehusika katika maandalizi na uendeshaji wake.

Mnyika ameeleza hayo leo, Ijumaa, Agosti 28, 2026, katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, wakati akietoa ushahidi wa utetezi katika kesi dhidi ya Lissu.

Lissu, ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu na mahakama za chini yake, anakabiliwa na shtaka la kutishia Serikali kinyume na Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuchapisha maneno ya kuitisha Serikali.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Dunstan Ndunguru akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Mnyika abeba dhamana

Akiongozwa na Lissu katika kutoa ushahidi wake, Mnyika amesema nafasi yake kama Katibu Mkuu ni ya kiutendaji na kwamba, yeye ndiye mwenyekiti wa sekretarieti ya Chadema, chombo kinachotekeleza shughuli za kila siku za chama.

Amesema Chadema ina mikutano ya aina mbalimbali, ikiwamo ya ndani na ile ya kikatiba, ambayo maandalizi yake hufanywa na sekretarieti ya chama.

Kwa mujibu wa Mnyika, Sekretarieti hiyo inajumuisha katibu mkuu, ambaye ndiye mwenyekiti wake, naibu makatibu wakuu wawili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, pamoja na katibu wa sekretarieti anayeteuliwa na katibu mkuu.

Ametaja pia wakurugenzi wa kurugenzi mbalimbali za chama, wataalamu na makatibu wa mabaraza ya chama, yakiwemo Baraza la Wazee (Bazecha), Baraza la Wanawake (Bawacha) na Baraza la Vijana (Bavicha).

Amesema mwenyekiti wa Chadema si mjumbe wa sekretarieti ya Taifa na kwa kawaida hashiriki vikao vya sekretarieti hiyo.

Katika ushahidi wake, Mnyika amekanusha madai ya Jamhuri kwamba Aprili 3, 2025, Lissu ndiye aliyeitisha mkutano wa watia nia wa Chadema waliokuwa wamekusudia kugombea ubunge na nafasi nyingine katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Badala yake, amesema yeye ndiye aliyekuwa na jukumu la maandalizi ya mkutano huo kwa kila hatua.

“Mkutano huo ulikuwa wa ndani wa chama na ulifanyika katika makao makuu ya Chadema, Mikocheni, Mtaa wa Daima. Uliwahusu waliokuwa na nia ya kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, maarufu kama watia nia,” amesema.

Amesema wazo la kufanya mkutano huo lilitoka kwake na uliandaliwa kupitia maelekezo aliyoyatoa katika vikao vya sekretarieti, ambako majukumu ya maandalizi yaligawanywa.

Mnyika amesema pia aliridhia fedha za matumizi ya mkutano huo akiwa ofisa masuhuli na kwamba alishiriki katika mkutano wenyewe.

Mnyika amesisitiza kuwa Lissu hakuhusika katika maandalizi ya mkutano huo wala kuwaalika watia nia na waandishi wa habari.

“Mwenyekiti wa chama hakushiriki kwa namna yoyote katika maandalizi ya mkutano huo. Mwenyekiti hakushiriki kwa namna yoyote kuwaalika ama watia nia au waandishi wa habari,” amesema.

Amesema mkutano huo ulikuwa sehemu ya uhamasishaji wa utekelezaji wa azimio la Mkutano Mkuu wa Chadema la kutaka kufanyika kwa mabadiliko na mageuzi ya kikatiba na kisheria yatakayowezesha kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki, chini ya kaulimbiu ya No Reforms, No Election.

Kwa mujibu wa Mnyika, mbali na watia nia, viongozi wakuu wa chama walioalikwa kwenye mkutano huo walikuwa Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara, John Heche na Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar, Said Mzee Said.

Amesema jukumu la kuwaalika waandishi wa habari lilifanywa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, Brenda Rupia.

Mnyika ameeleza kuwa alimwelekeza Rupia kutoa taarifa kwa umma kuhusu kufanyika kwa mkutano huo, ambapo taarifa hiyo ilitolewa Machi 27, 2025 ikiwa imesainiwa na Rupia.

Amesema wakati huo Lissu alikuwa katika ziara ya Kanda ya Nyasa, iliyohusisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa na Rukwa, kwa ajili ya kampeni ya No Reforms, No Election, iliyoanzia Mbeya Machi 23, 2025.

Mnyika amesema vyombo vya habari alivyovikumbuka vilivyokuwepo kwenye mkutano huo ni Jambo TV, The Chanzo na Mwanzo TV.

Amesema waandishi hao walialikwa kwa lengo la kutumia uhuru wao wa habari kuripoti madai ya Chadema kuhusu mabadiliko ya kisheria na kikatiba, yatakayowezesha kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki.

Ameongeza kuwa wakati wa kuwaalika waandishi wa habari, hawakupewa maelekezo kuhusu vifaa walivyopaswa kuja navyo wala namna ya kutumia kamera zao.

Pia amekanusha madai kwamba Lissu ndiye aliyesambaza video inayomwonyesha akitoa hotuba yenye maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini.

Mnyika amesema kabla ya mkutano huo alieleza kuwa ungekuwa na sehemu mbili, ambapo sehemu ya kwanza ingeihusisha waandishi wa habari na sehemu ya pili isingewahusisha.

Kwa mujibu wake, katika sehemu ya kwanza viongozi wa chama walitoa hotuba fupi, akiwemo yeye mwenyewe, manaibu katibu wakuu wa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara, John Heche.

Amesema Lissu alitoa hotuba ndefu iliyochukua takribani saa mbili.

“Lengo la kuwaalika waandishi wa habari kwenye sehemu hiyo lilikuwa ni kutumia uhuru wao kuchukua habari na kuzifikisha kwa umma kuhusu madai yetu ya mabadiliko ya kisheria kuwezesha uchaguzi huru na wa haki, chini ya kaulimbiu ya No Reforms, No Election,” amesema.

Baada ya kueleza hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu, Agosti 31, 2026 na Mnyika ataendelea na ushahidi wake wa msingi.

Baada ya kukamilisha ushahidi wake wa msingi, anatarajiwa kuhojiwa na waendesha mashtaka kuhusu maelezo atakayokuwa ameyatoa katika ushahidi wake.

Lissu ahitimisha ushahidi

Kabla ya Mnyika kutoa ushahidi, Lissu Lissu, amehitimisha ushahidi wake wa msingi katika kesi hiyo, kwa kufafanua baadhi ya majibu ya maswali aliyoulizwa na waendesha mashtaka.

Hata hivyo, hatua hiyo iliambatana na mapingamizi ya mara kwa mara kutoka kwa upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga.

Katuga alipinga baadhi ya maelezo akidai Lissu alikuwa akitoa ushahidi mpya au kufafanua mambo ambayo tayari yalijibiwa. Baadhi ya mapingamizi yalikubaliwa na mahakama, huku Lissu akitakiwa kuzingatia mipaka ya hatua hiyo.

Lissu alianza ushahidi Agosti 21, baada ya mahakama kumkuta ana kesi ya kujibu kutokana na ushahidi wa mashahidi 17 wa Jamhuri. Katika siku tatu za ushahidi wa msingi, alikanusha tuhuma na kuhoji ubora wa ushahidi na upelelezi wa kesi hiyo.

Схожие новости

#Наименование новостиТональностьИнформативностьДата публикации
1Lissu alivyohitimisha utetezi wake katikati ya mapingamizi ya Jamhuri08.2628-08-2026
2Ijue siri ya kisukari iliyojificha kwenye wali, ugali01007-08-2026
3Dk Nchimbi alivyopigwa chenga ya mwili01028-08-2026
4Kilio cha abiria Stendi ya Magufuli chaanza kutatuliwa01028-08-2026
5Migogoro inapogeuka rafiki wa ndoa01009-08-2026
6Serikali yataja sababu ya kuja na chanjo ya polio08.2628-08-2026
7Aliyedaiwa kuchoma moto mahakama Moshi akamatwa kwenye Maulidi01026-08-2026
8Warioba aeleza wasiwasi wake kupatikana Katiba mpya 202902028-08-2026
9Mashindano ya Feassa yafunga shule Morogoro Mjini, ikiibua sintofahamu01010-08-2026
10Liga bakom grova stölder – flera dalaorter drabbade0527-12-2025

Классификация: . Схожих патентов: 0. Схожих новостей: 10. Тональность: 0. Информативность: 10. Источник: www.mwananchi.co.tz.