Soma zaidi...
Dar es Salaam. Licha ya Dk Emmanuel Nchimbi kufukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wachambuzi wa siasa wamesema hatua hiyo haipaswi kutafsiriwa kuwa mwisho wa safari yake ya kisiasa ndani au nje ya vyama vya siasa.
Wamesema historia ya siasa za Tanzania inaonesha wapo viongozi waliowahi kufukuzwa au kuondoka kwenye vyama, lakini baadaye wakarejea na kuendelea kushiriki shughuli za kisiasa.
Taarifa ya kufukuzwa kwa Dk Nchimbi ilitangazwa Agosti 26, 2026, na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, baada ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa vilivyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Migiro alisema vikao hivyo vilijadili suala la nidhamu na maadili lililokuwa linamkabili Dk Nchimbi na, baada ya kuzingatia taarifa mbalimbali, viliridhika kuwa Katiba ya CCM ilikuwa imekiukwa.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku moja bada ya Dk Nchimbi kuwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais kwa Rais Samia, ambaye alikubali ombi hilo.
Huenda isiwe mwisho
Akizungumzia mustakabali wa kisiasa wa Dk Nchimbi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Onesmo Kyauke, amesema bado ni mapema kuhitimisha kuwa safari yake ya kisiasa imefikia kikomo.
Amesema Dk Nchimbi ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa na umri unaomruhusu kuendelea kushiriki masuala ya kisiasa au ya umma kwa namna mbalimbali katika miaka ijayo.
Kwa mujibu wa Dk Kyauke, kufukuzwa uanachama hakufungi milango yote, kwa sababu bado kuna uwezekano wa kuomba msamaha na kurejeshwa ndani ya chama, endapo vikao husika vitaona inafaa.
Ametolea mfano wa Bernard Membe (hayati) na baadhi ya wanachama wengine waliowahi kufukuzwa, lakini baadaye wakarejeshwa baada ya kufuata taratibu zilizowekwa na chama hicho tawala.
“Bado ni kijana kisiasa na amekuwa katika mfumo wa siasa kwa muda mrefu. Hii haimaanishi safari yake imekwisha, kwa sababu mazingira yanaweza kubadilika,” amesema Dk Kyauke.
Mbali na uwezekano wa kurejea CCM, amesema Dk Nchimbi anaweza kuamua kubaki nje ya vyama vya siasa na kushiriki masuala ya kitaifa kupitia njia nyingine.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Revocatus Kabobe, amesema kufukuzwa kwa Dk Nchimbi kunabadilisha namna wengi walivyoutazama uamuzi wake wa kustaafu siasa.
Amesema awali kulikuwa na mtazamo kwamba kujiuzulu kwake kulitokana na uamuzi binafsi wa kuhitimisha maisha ya kisiasa, lakini kufukuzwa kunatoa tafsiri nyingine ya tukio hilo.
Amesema viongozi wengi duniani wamewahi kuondoka katika nafasi za kisiasa na baadaye kuendelea kutoa mchango kupitia ushauri, diplomasia, taasisi za utafiti au mashirika ya kijamii.
Hata hivyo, Dk Kabobe amesema pia kuna uwezekano wa Dk Nchimbi kutafakari upya msimamo wake baada ya muda na kuamua kurejea katika ulingo wa siasa kwa namna tofauti.
“Kufukuzwa kwake kunaweza kuwa mwanzo wa kipindi cha kujipanga upya, kujenga taswira mpya mbele ya umma na kuamua hatua za baadaye,” amesema.
Naye, mchambuzi wa siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Salbinus David, amesema tukio hilo linaweza kuwa na athari katika namna Dk Nchimbi atakavyopanga maisha yake ya kisiasa.
“Kufukuzwa kutoka chama tawala ni tukio kubwa kisiasa ambalo huacha alama katika historia ya mwanasiasa, hivyo linaweza kuathiri maamuzi yatakayofuata,” amesema.
Jaji Warioba
Wakati wachambuzi wakitoa mitazamo yao, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amefichua mazungumzo aliyofanya na Dk Nchimbi kabla na baada ya kujiuzulu.
Jaji Warioba amesema baada ya kuona taarifa ya kujiuzulu kwa kwake, alimtafuta kwa simu ili kuthibitisha kama taarifa iliyokuwa ikisambaa ilikuwa ya kweli.
Amesema Dk Nchimbi alimthibitishia kuwa taarifa hiyo ilikuwa yake na kwamba walizungumza pia kuhusu hatua mbalimbali zilizokuwa zimechukuliwa kuhusiana na suala hilo.
“Nilipoona taarifa nikampigia simu, akanijulisha ni yake. Tukazungumza kama ameshapata uamuzi wa Rais kuhusu ombi lake la kujiuzulu,” amesema Jaji Warioba.
Amesema baadaye alipata taarifa kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa ameridhia ombi hilo kwa mujibu wa taratibu zinazotakiwa, hata alipojaribu tena kuwasiliana naye simu zake hazikupokelewa na ujumbe aliotuma haukujibiwa.
Aidha, amesema kabla ya matukio hayo, Dk Nchimbi aliwahi kumtembelea na walijadiliana masuala mbalimbali ya kitaifa yaliyokuwa yakigusa mustakabali wa nchi.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, moja ya mambo makubwa aliyomshauri Dk Nchimbi ni umuhimu wa kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.
Amesema changamoto nyingi zinazoonekana katika mfumo wa kisiasa na kiutawala zinaweza kupata ufumbuzi wa kudumu iwapo mchakato huo utakamilishwa.
“Nilimshauri kwamba matatizo mengi tuliyonayo yanatokana na kutokamilika kwa mchakato wa Katiba mpya, hivyo suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele,” amesema.
Akizungumzia uamuzi wa chama, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed, maarufu Dimwa, amesema wanaunga mkono uamuzi uliofikiwa na vikao vya juu.
Amesema Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ni vyombo halali vya chama na kwamba uamuzi wake unapaswa kuheshimiwa na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla.
Anaweza kurudi CCM
Hata hivyo, kufukuzwa uanachama kwa Dk Nchimbi hakumfungii milango ya kuwa mwanachama tena wa CCM, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na kanuni za uongozi na maadili za chama.
Ana njia mbili za kurudi kwenye chama chake. Moja, inafafanuliwa na Kifungu cha 8 cha Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, kinachompa haki ya kukata rufaa kama hakuridhishwa na adhabu iliyotolewa kwa makosa ya ukiukwaji wa maadili.
“Mwanachama au kiongozi yeyote ambaye hataridhishwa na adhabu iliyotolewa kwa makosa ya ukiukwaji wa maadili atakuwa na haki ya kukata rufaa kwa kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,” inaeleza kanuni hiyo.
Njia ya pili imeelezwa katika Ibara ya 13(3) ya Katiba ya CCM. Kwa mujibu wa ibara hiyo, mwanachama aliyefukuzwa uanachama anapotaka kujiunga, itabidi aombe upya na atapeleka ombi lake ama katika Halmashauri Kuu ya Wilaya au kikao kilichomfukuza.
“Mwanachama aliyeachishwa au kufukuzwa uanachama akitaka kujiunga tena katika CCM, itabidi aombe upya, na atapeleka maombi yake hayo ama katika Halmashauri Kuu ya Wilaya ama kikao kilichomwachisha au kumfukuza uanachama,” imeeleza.
Njia hiyo ilitumiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CCM Tanzania (UWT), Sophia Simba, alipofukuzwa uanachama Machi, 2017 kwa makosa ya usaliti katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Baada ya kufukuzwa, Novemba 2017, alimwandikia barua Mwenyekiti wa CCM Taifa wa wakati huo, hayati John Magufuli, ya kuomba msamaha na kuomba uanachama upya.
Magufuli aliwasilisha ombi la Sophia mbele ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), nacho kikaridhia kumsamehe na kumrejeshea uanachama wake.
| # | Наименование новости | Тональность | Информативность | Дата публикации |
|---|---|---|---|---|
| 1 | Ndejembi awakuna wadau, apewa angalizo | 0 | 10 | 27-08-2026 |
| 2 | Hivi ndivyo Dk Nchimbi anavyoweza kurudi CCM | 0 | 10 | 27-08-2026 |
| 3 | Utata ukomo umakamu wa rais wa Nchimbi, wanasheria watofautiana | 0 | 8.4 | 27-08-2026 |
| 4 | Bunge kumthibitisha Ndejembi leo | 0 | 10 | 28-08-2026 |
| 5 | Jaji Warioba afichua alichozungumza na Dk Nchimbi kabla, baada ya kujiuzulu | 0 | 10 | 27-08-2026 |
| 6 | Zacharia: Mhitimu la saba anayetamba kwenye uhandisi | 0 | 10 | 25-08-2026 |
| 7 | Ijue siri ya kisukari iliyojificha kwenye wali, ugali | 0 | 10 | 07-08-2026 |
| 8 | Migogoro inapogeuka rafiki wa ndoa | 0 | 10 | 09-08-2026 |
| 9 | Chanzo ghorofa kupigwa mnada kwa mkopo wa Sh10 milioni | 0 | 5 | 20-07-2026 |
| 10 | UWT: Hakuna mwanachama aliye juu ya CCM | 0 | 10 | 28-08-2026 |